Ufanye Nini Unapoumizwa Moyo Na Watu Wako Wa Karibu/ Jinsi Ya Kupokea Uponyaji kwa Moyo Ulioumizwa
Ikiwa umeshindwa kuulinda moyo wako kwa sababu ya kuzidiwa
na mambo magumu na mabaya sana; usikate tamaa, bado tumaini lipo. Wengi hudhani
kwamba upako wa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kuhubiri habari njema na kuombea
wagonjwa tu. Lakini Neno la Mungu linaonyesha wazi kwamba kuna upako wa kuganga
mioyo iliyovunjika. Isaya 61:1 inasema, “Roho ya Bwana Mungu i juu yangu;
kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma
ili kuwaganga waliovunjika moyo.” Lipo tumaini la
kupata uponyaji wa moyo uliovunjika. Kama Neno la Mungu linavyosema. Upo upako
wa kuganga moyo uliovunjika. Uponyaji wa moyo ulioumizwa huambatana na uponyaji
wa magonjwa yanayotokana na kuumizwa moyo. Njia zifuatazo zinaweza kukusaidia
kupata uponyaji wa moyo wako
1. Kumwomba Mungu
Kama vile mgonjwa anavyomwomba Mungu kwa ajili ya uponyaji
wa magonjwa, ndivyo unaweza kumwomba Mungu akuponye moyo wako. Kuna upako
maalum wa kuponya mioyo iliyoumia. Haijalishi umeumizwa kiasi gani, Mungu ana
uwezo wa kukuponya. Zaburi 147:3 inasema, “Huwaponya waliopondeka
moyo na kuziganga jeraha zao.”
Jitahidi upate muda wa kutulia mbele za Mungu katika kuomba
na kufunga. Hakika Mungu ni mwaminifu atakuponya moyo wako na magonjwa
yanayotokana na kuumizwa moyo. Zaburi 34:15, 18, 19 inasema, “Macho
ya BWANA huwaelekea wenye haki, na masikio yake hukielekea kilio chao. 18 BWANA
yu karibu nao waliovunjika moyo na waliopondeka roho huwaokoa. 19 Mateso ya
mwenye haki ni mengi, lakini BWANA humponya nayo yote.”
2. Kufanyiwa Ushauri na Maombezi
Unaweza kupokea uponyaji wa moyo kwa njia ya ushauri na
maombezi. Kupitia ushauri unaweza kufanyiwa maombi ya kufunguliwa kutokana na
pepo wa uchungu na kutokusamehe. Yakobo 5:16 inasema,“Ungameni dhambi
zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki
kwafaa sana akiomba kwa bidii.” Usifiche uchungu moyoni mwako. Kwa
maana ukificha uchungu moyoni utapata magonjwa. Hakikisha unashughulikia
machungu yaliyo moyoni mwako. Mithali 28:13 inasema, “Afichaye
dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”
3. Kunena kwa Lugha kwa Muda Mrefu
1 Wakorintho14:4 inasema, “Yeye anenaye kwa lugha
hujijenga nafsi yake.” Mambo mengine tunayoyapitia hudhoofisha
mioyo au roho zetu. Kwa njia ya kunena kwa lugha, roho yako inaweza kupokea
nguvu mpya kutoka kwa mungu.
Lakini inategemea ni kwa muda gani unaokaa kwenye
maombi ya kunena kwa lugha. Mfano wa kujijenga nafsi ni kuchaji simu. Mtu
anayechaji simu kwa dakika mbili ni lazima simu itaanza kuzimika baada ya muda
mfupi tu. Lakini mtu anayechaji simu yake kwa muda mrefu kama masaa matatu simu
yake itakuwa na nguvu ya kutumika kwa muda mrefu bila kuzimika. Je wewe
unatumia muda gani kujichaji kiroho? Ukijichaji kiroho kwa muda mfupi, ni
rahisi kuishiwa nguvu za kiroho. Unapokuwa na nguvu kidogo inakuwa vigumu
kustahimili mawimbi ya kiroho, hivyo inakuwa rahisi kuumizwa moyo.
Jizoeze kunena kwa lugha kwa muda mrefu. Hata kama ulikuwa umeumizwa moyo, Roho
Mtakatifu atakuhuisha na kukupa nguvu za kuyaachilia yale yaliyokuumiza moyo.
4. Kutafakari na kukiri Neno la Mungu
tumia muda mwingi ukitafakari na kulitamka Neno la Mungu.
Mithali 16:24 inasema, “Maneno yapendezayo ni kama sega la asali;
ni tamu nafsini, na afya mifupani.” Unapokiri na kutafakari Neno
la Mungu, moja kwa moja mifupa yako hupata dawa. Kwa maana maneno yapendezayo
ni afya mifupani.
Pia kuna ahadi ya Mungu ya kukuondolea yasiyofaa moyoni
mwako na kukupa furaha iliyo kamilifu. Isaya 61:3 inasema, “Kuwaagizia
hao waliao katika Sayuni wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha
badala ya maombolezo, na vazi la sifa badala ya roho nzito.” Tafakari
jinsi Bwana alivyokuandalia taji ya maua, yaani kibali badala ya kukataliwa.
Bwana atakupa furaha itakayobubujika toka kwenye vilindi vya moyo. Badala ya
kuwa mtu wa huzuni atakuvika vazi la sifa, nyimbo zitabubujika toka moyoni
mwako. Jitamkie kibali, jitamkie mafuta ya furaha, jitamkie vazi la sifa. Kwa
maana Mithali 15:4 inasema, “Ulimi safi ni mti wa uzima; bali
ukorofi wa ulimi huvunja moyo.”
5. Tumia Muda Wako Kukamilisha Malengo Yako
Usipoteze muda wako kwa kukata tamaa na kusononeka. Badala
yake tumia muda wako kukamilisha malengo ambayo umejiwekea katika maisha yako.
Usimpe ibilisi nafasi ya kuvuruga malengo yako. Nia ya Ibilisi ni kutaka
kukukatisha tamaa ili ushindwe kufanikisha malengo yako. Hakikisha unampinga na
kuendelea na mpangilio wa shughuli zako kana kwamba hakuna kilichotokea.
Kwa muda mrefu nilipitia mambo magumu ambayo yaliniumiza
sana moyo wangu. Kuna watu ambao shetani aliwainua ili kuharibu kusudi la Mungu
katika maisha yangu. Kwa muda mrefu nikawa najitahidi kuwasamehe na kuanza
kufanya kazi ya Mungu. Mara nilipopata mpenyo waliinuka na jambo jingine la
kuniumiza zaidi. Ndipo mtumishi wa Mungu kutoka Marekani mtume Greg Howse
akanitolea unabii kwamba, “Mungu anasema, nakuponya moyo wako,
nakuponya hisia zako kwa maana watu wengi wamekunenea maneno ya kukuumiza moyo
wako. Nitakufanya mwanamke mwenye afya, nitakufanya mtumishi mkubwa na upako wa
Deborah utakuwa juu yako.” Pamoja na kwamba shetani aliendelea
kuwatumia watu wengine kunisema vibaya na kunisingizia kila neno baya, niliamua
kuchukua hatua ya kukubaliana na wazo la Mungu juu ya maisha yangu.
Hakika Bwana aliuponya moyo wangu. Nikasamehe kabisa!! Kisha
nikaamua kutoyaangalia mambo ambayo shetani aliyatumia kunivuruga kwa kuwatumia
wale watu. Badala yake nikaamua kufanya bidii kutenda yale niliyoitiwa.
Kama ningeyaangalia mapito yangu, nisingefanyika baraka
kwenye Mwili wa Kristo. Uvumilivu ni tunda la Roho ambalo kila Mkristo anapaswa
kuwa nalo. Uvumilivu ni kuendelea mbele bila kubadilika hata kama unapitia
mambo magumu. Uvumilivu ni sifa ya mtu anayempenda na kumcha Mungu. Katika
uvumilivu mwingi Mungu amenifundisha siri ya kulinda moyo na kupokea uponyaji
wa moyo.
6. Kuwekewa Mikono
Bwana alinifunulia juu ya upako wa kuganga mioyo iliyoumia
kama tunavyosoma katika Isaya 61:1 inasema, “Roho ya Bwana Mungu i juu
yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari
njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo.” Ndipo
nilipojifunza kuachilia upako huo kwa watu waliovunjika mioyo yao. Upako wa
Roho Mtakatifu sio wa kuhubiri na kuponya magonjwa tu; bali ni pamoja na
kuganga mioyo iliyoumizwa. Kwa hiyo unaweza kuwekewa mikono na watumishi wa
Mungu kama vile unavyoweza kuwekewa mikono wakati unapoumwa.
7. Kusamehe na Kuchukuliana
Chanzo kikubwa cha kuumizwa moyo ni kushindwa kusamehe. Kusamehe
ni msingi wa maisha ya kila Mkristo. Kwa maana mtu akishindwa kusamehe,
anatembea nje ya Neno la Mungu. Baada ya kushindwa kusamehe, uchungu wa moyoni
huufanya mwili kuzalisha kemikali ambazo huleta madhara katika mwili. Mithali
11:17 inasema, “Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; aliye mkali
hujisumbua mwili wake.” Kwa faida ya roho yako na mwili wako
inakupasa kusamehe. Kusamehe ni uamuzi, ukiamua kusamehe itakuwa rahisi kuondoa
uchungu moyoni. Lakini usiposamehe ni rahisi kuingiwa na mapepo ya uchungu
ambayo yatakufanya ujisikie uchungu zaidi. Mapepo ya uchungu huambatana na
mapepo ya udhaifu ambayo hushambulia mwili. Watu wengi waliookoka hufungulia
milango ya mapepo ya uchungu na mapepo ya udhaifu. Mapepo hayawezi kumwingia
mtu aliyeokoka bila sababu. Mithali 26:2 inasema, “Kama shomoro
katika kutangatanga kwake, na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; kadhalika
laana isiyo na sababu haimpigi mtu.” Hata kama umeonewa, inakupasa
usamehe kwa ajili ya usalama wako kiroho na kimwili. Ninajua kwamba wapo watu
wasiotaka suluhu kiasi kwamba hata kama wamekosa hawaoni sababu ya kutubu.
Lakini unapaswa kuamua kumsamehe mtu wa jinsi hiyo kwa maana ndiyo mapenzi ya
Mungu na afya ya mwili wako. Fanya jitihada ya kutengeneza na wale wote ambao
hamkuelewana. Pia ujifunze kuchukuliana na mapungufu ya watu wengine.
8. Kusifu na kuabudu
Kumsifu Mungu kwa kumaanisha na kumwabudu Mungu katika roho
na kweli yaani unapoabudu kwa kumaanisha kama vile uko kwenye maombi ya ndani
huondoa uchungu moyoni na kuleta furaha ya Roho Mtakatifu. Watu wengi
hawajihusishi na kusifu na kuabudu kwa kudhani kwamba huo ni wajibu wa
waimbaji. Waimbaji ambao husimama mbele ni viongozi wa kukusaidia wewe ili
uweze kusifu na kuabudu inavyokupasa. 2 Wafalme 6:14 inasema, “Daudi
akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya
kitani.” Mfalme Daudi alicheza mbele za BWANA akijua kuwa BWANA
ndiye Mfalme mkuu. Ukilitambua hili utamsifu Mungu kwa nguvu zako zote na
kumwabudu kwa moyo wako wote. Watu wengi hupokea uponyaji wa mioyo na miili yao
kwa njia ya kusifu na kuabudu.
Comments
Post a Comment