I KUMPENDA MUNGU KWA VYOTE BILA KUBAKIZA CHOCHOTE KAFARA YA YESU:

 IMANI NI ITIKIO LA SHUKRANI LA MOYO WA UPENDO KWA MUNGU KWA  UPENDO WAKE ALIOUONYESHA KWETU PALE MSALABANI. 

NI KUMPENDA  MUNGU KWA VYOTE BILA KUBAKIZA CHOCHOTE  KAFARA YA YESU:



Mara nyingi ni rahisi kwetu kuiangalia kafara ya Kristo kwa tukio la msalabani tu, yaani Kalvari.
Lakini hebu tutafakari maneno ya Wafilipi 2:5-8, “kuweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo
ilikuwemo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye
hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana
utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana anaumbo
kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba” Maneno haya
yanatupatia sura halisi ya kile ambacho dhambi ilikisababisha kwa Uungu.
Bwana Yesu, ambaye neno la Mungu linasema ni Mungu, yaani ni mmoja wa nafsi za Uungu,
alifanyika mwili, yaani alitwaa ubinadamu (soma Yohana 1:14,18). Jambo hili kwa kweli ni zaidi ya
akili zetu kulipima na kulielewa jinsi lilivyofanyika. Mungu kutwaa ubinadamu, akazaliwa kama
mtoto mchanga wa kibinadamu! Ajabu kwa akili zetu za kibinadamu. Soma Mathayo 1:18-23, Luka
1:26-37; 2:4-14. Kwa hiyo tunaweza kuona ukuu wa kafara ya Bwana Yesu kwa kutambua kuwa
yeye ni Mungu, lakini “hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho” (Wafilipi
2:6b). Isije ikafikiriwa kuwa kwa kufanya hivyo Yesu aliudharau Uungu wake. La, bali inaonyesha
ni kwa kiasi gani mwanadamu ni wa thamani mbele za Mungu. Na kama mwanadamu yeyote
atafanya dharau kwa Bwana kwa kufikiria hivyo atakuwa anafanya kosa kubwa sana. Kwa hiyo
muumbaji aliyemuumba mwanadamu, akajishusha ili kutuokoa. Kwa hiyo tangu nia ilipokuwamo
ndani yake na akajitoa ili atuokoe, tayari kile kilichofanyika msalabani kilikuwa kimeanza - Yaani
Mateso.
Ubinadamu wa Yesu:
Unajua, tatizo letu kuu wanadamu ni kutoamini, yaani kutomwamini Mungu. Na unajua hili ndilo
lilikuwa hasa jaribu la shetani kwa Hawa, na ndio msingi wa majaribu yake yote kwetu. Sasa kwa
sababu hiyo, hata kile ambacho Mungu amesema katika neno lake, ni vigumu sana kukiamini; na
mojawapo ni kuhusu Ubinadamu wa Yesu. Wengi wetu tumeendelea kuamini kuwa Bwana Yesu
hakutwaa mwili hasa, yaani hakuwa mwanadamu kama sisi, na kwa jinsi hiyo hata kile alichofanya
katika hali yake ya ubinadamu hakina uzito sana maana inaonekana kana kwamba ni kiini macho tu.
Hebu tuone neno la Mungu linavyosema. Labda, kwa kuanzia, tuone kile Isaya anachosema (Isaya
9:6). “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume: Na uwezo wa kifalme
utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa
Milele, Mfalme wa amani”. Kama nilivyotangulia kusema, mtu yeyote anayefanya dharau juu ya
ubinadamu wa Bwana Yesu anafanya dhambi kubwa. Unapotafakari maneno ya fungu hilo
yanaonyesha wazi kuwa, ijapokuwa mtoto huyu anayezaliwa ni mwanadamu, tena mwanamume,
lakini bado anaitwa, Mshauri, Mungu, Baba na Mfalme! Cheo chake cha uungu kiko palepale. Sasa,
kuna watu ambao wanamchukulia Bwana Yesu kama wao wenyewe, (sisemi kama mwanadamu, bali
kama wao wenyewe) yaani, kile wanachofikiri, kusema au kutenda, ndivyo wanavyomfanya Kristo
awe. Lakini hili ni kosa. Ijapokuwa alitwaa ubinadamu, lakini aliishi maisha tofauti na sisi katika
16
kufikiri kwake, kusema kwake na kutenda kwake. Je, hii haionyeshi kuwa lazima angeishi tofauti na
sisi maana yeye ni Mungu? La, yeye mwenyewe alisema “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe
ila lile ambalo amwona Baba analitenda ----” (Yohana 5:19). “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe
----” (Yohana 5:30), “kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali
mapenzi yake aliyenipeleka” (Yohana 6:38). Ndio maana, kama mwanadamu yeyote, alihitaji
msaada wa Mungu. Ndio maana alijazwa Roho Mtakatifu, na Roho ndiye akawa kiongozi wake
(soma Mathayo 3:16, 4:1). Tofauti ya ubinadamu wake iliyo wazi ni kuwa - daima siku zote, Yesu
alitii uongozi wa roho Mtakatifu - alifanya mapezi ya Mungu (soma Yohana 8:28-29). Hakutenda
dhambi (soma Waebrania 4:15) na hakuwa na uadui na Mungu. Ndani yake asili mbili ziliunganika.
Jambo la msingi kufahamu ni kuwa ili ukombozi wetu ufanyike, ilikuwa lazima Yesu kutwaa
ubinadamu. Kwani, kama vile Mungu alivyoumba wanadamu wote katika au ndani ya Adamu (soma
Matendo 17:26), Vivyo hivyo katika mpango wa ukombozi alituunganisha sote (ubinadamu wote)
ndani ya Kristo (soma Waefeso 2:16). Kwa hiyo tendo la Bwana Yesu kufanyika mwili, ni
kuunganisha wanadamu wote ndani ya uungu, na ndio “Imanueli” yaani “Mungu pamoja nasi”
(Mathayo 1:23). Ni kwa kutambua na kulipokea neno moyoni, ndipo kafara ya Kristo inapoleta sura
halisi katika ufahamu wetu, maana kufanyika kwake mwanadamu kumetufungamanisha naye kama
ndugu yetu (soma Waebrania 2:11). Kristo hakufanya badala yetu, bali kwa ajili yetu. Ndiyo maana
hakuna chochote tunachoweza kufanya nje ya Kristo kwa ajili ya wokovu wetu, maana nje yake,
tunakuwa katika utu wetu wa kale ambao hauwezi kumtii Mungu (soma Waruni 7:14, 1 Kor. 2:14).
Lazima Kristo awe ndani yetu nasi ndani yake kwa imani.
Muhimu: Kwa sababu haikuwezekana kabisa katika hali yetu ya dhambi kuitenda na kuitimiza
haki ya Mungu, ndiyo maana kristo alitwaa mwili ili katika Yesu yote yawezekane.
Warumi 8:3-4 inasema, “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile
ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu , kwa kumtuma Mwanawe
mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi,
aliihukumu dhambi katika mwili, ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi,
tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” Kwa hiyo
ubinadamu wa Yesu umefanya iwezekane kwetu wanadamu kutimiza mapenzi ya
Mungu katika Kristo. Hapo nyuma tuliona kuwa kristo Yesu amefanya yote
yaliyopaswa kwa ajili yetu na si badala yetu. Ndiyo maana, kumpokea au
kumwamini yeye, ni kujisalimisha kwake ili atimize kusudi lake ndani yetu (soma
Wafilipi 2:13). Kwa hiyo yale tunayoweza kutenda tunapoamini, hayatakuwa yetu
sisi, bali ni Kristo atakayekuwa akitenda ndani yetu (soma Yohana 15:1-5). Hivyo
kujisifia matendo hayo ni kutwaa utukufu wa Mungu, maana pasipo yeye sisi
hatuwezi kufanya neno lolote. Kumpokea Yesu moyoni ni kufanya awe Mungu
(mtawala) wa maisha badala ya nafsi kuwa Mungu.
Kuzaliwa: Malaika akasema “maana leo katika mji wa Daudi, amezaliwa, kwa ajili
yenu, Mwokozi, ndiye kristo Bwana” (Luka 2:11). Ni kwa ajili yetu, Kristo alitwaa
mwili au ubinadamu, hivyo akazaliwa. Hivyo kuukubali ubinadamu wa Yesu ni
kuonyesha imani kwake kuwa - Uungu uliungana na ubinadamu,na hivyo kupokea
yote aliyofanya kwa ajili yetu. Kutoamini jambo hili ni kumkataa Kristo, na yote
aliyofanya hayatakuwa na faida yoyote kwa mhusika (soma 1 Yohana 4:2.3. Hapa,
katika kuzaliwa kwake ni mwanzo wa maisha yake hapa Duniani. Kupokea kwa
imani mwanzo huu ni kufungua moyo kupokea huduma yake ya maisha yake yote
yaliokuwa kwa ajili yetu.
Ubatizo: Kabla ya Bwana yesu kuanza kazi rasmi hapa duniani alibatizwa. Biblia inatuonyesha
kuwa Yesu hakuwa na dhambi (soma 1 Petro 2:22). Lakini Yohana mbatizaji
alikuwa akifanya ubatizo wa toba (soma Mathayo 3:6). Sasa kwa nini Yesu
alibatizwa kama hakutenda dhambi? Jibu alilolitoa yeye mwenyewe kwa Yohana ni
kuwa “kubali hivi sasa, kwa kuwa ndiyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Mathayo
3:15). Kwa kuliweka wazi jambo hili ni kuwa, kwa sababu Mungu aliwahesabu watu
kuwa ndani ya Kristo, hivyo dhambi zetu zilikuwa ndani yake. Hivyo alifanya toba
na kubatizwa kwa ajili ya dhambi zetu zilizokuwa ndani yake, yaani alizozibeba
(alitubeba ndani yake) (soma 2 Kor. 5:21, Isaya 53:6). Kwa jinsi hiyo ubatizo
tunaobatizwa una maana sana kuonyesha imani yetu kwa Yesu. Ndiyo maana,
17
kufanya kitu kingine kinyume na kile alichofanya Bwana, ni kumkataa yeye kama
haki yetu na tunajipatia haki yetu wenyewe, isiyo ya Mungu. Maandiko Matakatifu
yanasema hakuna wokovu katika mwingine awaye yote isipokuwa Kristo tu (soma
Matendo 4:12). Na kama tumeamini, ambako ni kujisalimisha kwake ili yeye atende
ndani yetu apendavyo, hakika atatuongoza kubatizwa kama yeye alivyofanya ili ile
haki ikamilike ndani yetu. Kufanya kitu kinyume, kama ubatizo, tofauti na ule wa
Yesu, ni sawa na sadaka aliyotoa Kaini ambayo haikuonyesha imani kwa Masihi
ajaye. Ni kutoamini. Ni kwa njia ya ubatizo (kuzamishwa majini) tunapoonyesha pia
kukubali mauti ya Kristo kwa ajili yetu, maana ubatizo ni kama ishara ya kuzikwa
naye, na kukubali kuifia dhambi pamoja naye; na mtu hazikwi kabla hajafa. Ni wazi
kuwa hii ni ishara ya kuonyesha imani yetu katika mauti yake (soma Warumi 6:2-5).
Ni haki kwa imani.
Maisha Aliyoishi:
Kama mwanadamu neno la Mungu linasema hivi kumhusu Kristo “---- bali yeye alijaribiwa
sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi” (Waebrania 4:15). Majaribu yote
yanayotupata, Bwana Yesu aliyapitia na akayashinda. Warumi 8.3 linasema, “---- na kwa sababu ya
dhambi aliihukumu dhambi katika mwili”. Yaani katika mwili ulio kama wako na wangu, Kristo
aliihukumu dhambi - maana yake aliishinda dhambi.
Yohana 8:29, “----kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo”.
Yohana 15:10, “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu, kama vile mimi
nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake”
Yohana 8:45, “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye kuwa nina dhambi”?
Kwa hiyo, maisha Kristo Yesu aliyoishi ya mwanadamu hapa duniani yalikuwa maisha ya utii kamili
kwa sheria za Mungu, ndiyo maana hakutenda dhambi. Na kwa sababu aliitii sheria kwa ukamilifu,
maandiko yanasema, “Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria ili kila aaminiye ahesabiwa haki”
(Warumi 10:4). Wengi wamelitafsiri fungu hili kumaanisha kuwa Kristo sasa ameondoa sheria na
hivyo hatupaswi kuzitii au kuzitenda. Lakini Bwana Yesu mwenyewe alisema “Msidhani ya kuwa
nalikuja kutangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Mathayo 5:17,19). Kwa
hiyo, maana ya Kristo kuwa mwisho wa sheria ni kuwa - yeye alitii sheria takatifu ya Mungu kwa
ukamilifu na hivyo sheria hiyo haimhukumu kuwa mkosaji. Sheria hiyo takatifu imeridhika kuwa
matakwa yake yametimizwa. Hivyo yeyote anayemwamini Yesu, yaani anayempokea Yesu moyoni,
hupewa uwezo wa kuzitii sheria za Mungu kwa ukamilifu - maana Kristo aliye ndani ya muumini
huyo huzitii sheria ndani yake na hivyo anasimama mbele za Mungu kama mtu mtakatifu, yaani
sheria haitamhukumu kuwa ameivunja. Kumbuka, si haki ya mtu binafsi, bali ni ya Kristo aliye ndani
yake (soma Rum. 8:1).
Mauti ya Msalaba:
Katika kitabu cha Wafilipi 2:8 tunasoma, “tena alipoonekana ana umbo kama mwadanamu,
alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti naam, mauti ya msalaba”.
• Waebrania 2:14 inasema, “Basi kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo
hivyo alishiriki yayo hayo ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti,
yaani Ibilisi”.
• Kwa nini mauti ilikuwa lazima kwa ajili ya ukombozi wetu? Ni kwa sababu ndiyo njia ambayo
kwayo Ibilisi angeharibiwa na nguvu zake. Kumbuka mwanzo 3:15 Kumponda kichwa yule
nyoka wa zamani. Ufunuo 12:11 “ Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na kwa neno la
ushuhuda wao ----“.
18
• katika maisha yake hapa duniani, daima Yesu Kristo alikabiliwa na vita vile vilivyoanzia kule
mbinguni. Ndani yake kulikuwa na mashindano makuu - atende kama mapenzi ya Baba yake
yalivyotaka ili mwanadamu aokolewe, au atende kama nafsi yake ilivyotaka ili ajiokoe mwenyewe
na mwanadamu apotee milele. Waebrania 12:2 linasema, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha
na kutimiza imani yetu, ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake, aliustahimili msalaba
na kuidharau aibu----.”
• Pale bustani ya Gethsemani Yesu aliomba kuwa “ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, walakini si
kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39). Alipokuwa mbele ya Pilato
alisema “----Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni
ili niishuhudie kweli----” (Yohana 18:37).
Mungu ashukuriwe. Kristo alistahimili msalaba, naam mauti ya msalaba. Pale msalabani Kristo
aliposubiliwa, Shetani alitoa matukano makuu kupitia kwa makutano waliokuwa pale ili ikiwezekana
Kristo ashuke msalabani na mwanadamu apotee milele - asiokolewe. Hebu soma jinsi ilivyokuwa
(Mathayo 27:40-44), “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako;
ukiwa ndiwe mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani
wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, aliokoa wengine, hawezi kujiokoa
mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.
Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka, kwa maana alisema, mimi ni mwana wa
Mungu. Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.” Maneno haya
makuu yakasemwa na wanadamu ambao ndio Kristo alikuja kuwaokoa!! Tusije tukawalaumu
Wayahudi hawa waliofanya hayo tukifikiri sisi ni wema kuliko wao. Kama wewe au mimi
tungekuwepo pale, yawezekana kabisa tungeshiriki kusema maneno hayo. Halafu pia, jambo la
muhimu kutambua na kukumbuka ni kuwa Bwana Yesu alikufa, si kwa ajili ya watu fulani tu, bali ni
kwa dhambi za ulimwengu wote. Dhambi zetu ndizo zilimsulibisha na kumuua (soma Isaya 53).
Maneno yaliyopigiwa msitari katika fungu hapo juu yanaonyesha vita kuu ambayo kila mwanadamu
amekuwa nayo na atakuwa nayo hadi mwisho.
Navyo ni vita dhidi ya nafsi. Unajua kama Yesu angeokoa nafsi yake, sisi sote tungepotea milele!!
Kama Mungu angemwokoa mwanawe pale msalabani asife, wewe na mimi ndio tungekufa kifo kile.
Lakini kwa Upendo mkuu usio na kifani, Mungu Baba akakaa kimya na mwana wake, Yesu, akafa
(soma Mathayo 27:46), ili wewe na mimi tuokolewe na kuurithi uzima wa milele. Kwa upendo huo
mkuu Kristo naye hakushuka msalabani kama shetani alivyotaka kupitia kwa wale makutano (soma
Warumi 5:6-8). Pamoja na yote hayo aliyofanyiwa, sikiliza alichosema Yesu; “Baba uwasamehe,
kwa kuwa hawajui watendalo----” (Luka 23:34). Upendo ulioje!!! Mwisho, Kristo alikufa msalabani
(soma Mathayo 27:50-54). Bwana Yesu hakuendelea kubaki kaburini. Siku ya tatu alifufuka (soma
Mathayo 28:1-6, Marko 16:1-6, Luka 24:1-6). Je, unajua Yesu Kristo amekufa msalabani ili tusije
tukafa mauti ya pili au ya milele katika jehanamu ya moto? Ni nini kitakuzuia usimpokee Yesu kuwa
Bwana na mwokozi wa maisha yako? Yeye alisema “aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini,
atahukumiwa” (Marko 16:16).
Kwa nini, basi, kuna dini au imani zinazofundisha kuwa Yesu Kristo si mwokozi na pia hakufa
msalabani? Jibu ni kuwa, ni kwa sababu yule adui, yaani Shetani aliamua kuwapoteza wanadamu
kupitia jina la dini. Kumbuka alipomdanganya Hawa hakumwendea moja kwa moja kama Shetani,
alimtumia nyoka na Hawa akadanganyika. Kama angewashawishi wanadamu kumkataa Mungu
kabisa, angegundulika kwa urahisi lakini sasa yeye hujifanya malaika wa nuru ili kunasa wanadamu
(soma 2 Wakorinto 11:13-15). Bwana Yesu ndiye ambaye Shetani anamchukia, lakini pia yeye Yesu
ndiye mwokozi. Hivyo Shetani atampinga kwa njia yoyote ile ili mpango wa Mungu usitumie.
Lakini Mungu ashukuriwe - Yesu ameshinda. Mpendwa msomaji, je, utamruhusu Kristo awe Bwana
na mwokozi wako, au nafsi yako mwenyewe? Kumbuka, Mungu asipotutawala na tukafanya
mapenzi yake, nafsi ndiyo itakuwa mungu kwetu na tutatenda kulingana na nafsi itakavyotuongoza.
Lakini kumbuka kuwa daima nafsi ina uadui na Mungu ndiyo maana ili kumfuata Yesu, lazima nafsi
isulibiwe (soma Luka 9:23-25, 14;26-27.
19

Comments

Popular posts from this blog

LINDA SAANA MOYO WAKO KULIKO VYOTE ULINDAVYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-I

VINYWA VYA MOYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-2

Ufanye Nini Unapoumizwa Moyo Na Watu Wako Wa Karibu/ Jinsi Ya Kupokea Uponyaji kwa Moyo Ulioumizwa