KUMBUKA, KUSUDILA MAISHA LIWE KUMTUKUZA MUNGU DAIMA.
Tofauti ya Haki Hizi:
Ili kutambua tofauti kati ya Haki kwa imani na Haki kwa matendo ya sheria, mtu hana budi kutambua
asili ya jambo lenyewe. Lakini kwa maelezo machache yanayoweza kutoa mwanga kuelewa jambo
lenyewe ni kuwa:
1. Haki kwa Imani - ni kitendo cha mwadanamu kukubali kupokea kwa njia ya imani kile
ambacho Mungu amemfanyia katika Kristo Yesu, kwa ajili ya wokovu wake. Na hii
huhusisha kuhesabiwa haki (Msamaha wa dhambi), haki ya Kristo kuwa maishani
(utakaso) (au kuiishi haki ya Kristo) na mwisho kuurithi uzima wa milele (kutukuzwa
pamoja na Kristo). Yaani tangu mwanzo hadi mwisho Mungu ndiye mtendaji kupitia
kwa Kristo na mwanadamu ni mpokeaji tu (kuamini).
2. Haki kwa Matendo ya sheria - hapa ni kitendo cha mwandamu kutumainia kile
alichotenda, anachotenda sasa na atakachotenda baadaye kulingana na sheria inavyotaka
atende, ili kujiokoa. Kwa hiyo mtu mwenyewe (nafsi) ndiyo mtendaji mkuu. Ndiyo
sababu ya dhana kuwa “Mungu anasaidia wanaojisaidia”. Lakini kama unakumbuka kile
Isaya 1:6 inachosema, utagundua kuwa kwa kweli mtu hana chochote anachoweza
kujisaidia mwenyewe maana amekufa (soma Waefeso 2:5). Sasa ni maiti gani inaweza
kufanya chochote? Hakika hakuna. Ndiyo maana kamwe haki hii binafsi haiwezi
kumpatia mwanadamu wokovu, yaani atoke dhambini na kuitimiza haki ya Mungu.
Haiwezekani kwani chochote anachofanya mtu hapo ni kwa sababu ya nafsi yake na wala
si kwa ajili ya utukufu wa Mungu aliye asili ya vyote tulivyo navyo.
IMANI:
Maandiko matakatifu yanasema “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya
mambo yasiyoonekana,” (Waebrania 11:1). “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa
maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu
wale wamtafutao,” (Waebrania 11:6).
Lakini imani ni nini pia. Ni mkono (Kiroho) wa mwanadamu wa kupokelea ahadi za Mungu. Yaani
ni kwa njia ya imani tu mwanadamu anaweza kupokea ahadi za Mungu kwake. Hivyo isieleweke
kuwa imani ndiyo mwokozi. La, bali ni njia yetu kuupokea. Na pia hiyo(imani) haitokani na sisi
wenyewe, bali ni kipawa cha Mungu (soma Waefeso 2:8-9, Waebrania 12:2). Imani ni msingi wa
maisha ya kumcha Mungu, maana amesema pasipo hiyo haiwezekani kumpendeza. Ndiyo maana
matendo ya haki tunayoweza kutenda, pasipo imani, bado ni machukizo tu. Yatakuwa hayajatimiza
ile kanuni ya mbinguni ya “Upendo usio na Ubinafsi:” Imani ni kumwamini Mungu kabisa kwa kila
jambo na kumtegemea yeye tu. Tunaweza kusema kuamini ni KUJISALIMISHA KWA MUNGU.
Mtu unapojisalimisha, huwa hakuna unachobakiza. Unajitoa kabisa kwa yule unayejisalimisha kwake
ili akutendee apendavyo. Ni hakika tunahitaji kujisalimisha kwa Mungu ili atutendee kama
apendavyo. Na tunafanya hivyo kwa kujua wazi kile anachotaka kutufanyia kwa kuwa yeye ni
14
mwaminifu, tofauti na ambavyo unaweza kufanya kwa mwanadamu anayebadilika-badilika. Imani
kwa Mungu ni jambo la hakika (soma Waebrania 11:1), sio bahati nasibu. Kwa kweli wanadamu
wengi sana tuna kitu kama bahati nasibu katika Ukristo wetu, wala hatuna hakika (imani) na Mungu.
Yaani tunafanya majaribio. Tukipata, bahati nzuri, tukipoteza au kukosa, bahati mbaya. Ukitaka
kuhakikisha ukweli huu, hebu jaribu kutafakari maombi yako mwenyewe na kile moyo wako ulicho
na uhakika nacho. Kwa mfano, unapoomba, ukaungama dhambi zako zote, na kueleza mengine
unayoyahitaji kwa Mungu, halafu unasema kwa jina la Yesu, Amina. Je moyoni mwako unaamini
(una hakika) kuwa ndivyo Mungu alivyofanya au atakavyofanya? Yaani Je, unaamini kuwa Mungu
amekusamehe kabisa dhambi zako na sasa anakuhesabu kuwa mwenye haki (mtakatifu) na kuwa sasa
hivi au saa hiyo hiyo tayari amekupatia uzima wa milele? Je, tunafanya maombi ili Bwana atutendee
mambo fulani, halafu mengine tutakamilisha wenyewe? Sasa kwa sababu hatuna hakika kuwa kwa
upande wetu tutafanya bila kukosea, basi hata Mungu tuna mashaka naye kama kweli atatenda kama
alivyoahidi. Ndiyo maana, kwa kweli, wengi wetu hatuna imani kwa Mungu wetu kwa kipimo cha
mbinguni. Tafakari swali la Bwana Yesu “---- Walakini, atakapokuja mwana wa Adamu, je! Ataiona
imani duniani,” ( Luka 18:8)? Bwana Yesu hakuwa anazungumzia dhana ya imani ambayo ndiyo
tuliyonayo watu wengi, lakini alikuwa akisema juu ya imani ya kweli ya Mungu (Haki kwa imani);
imani ya Yesu (soma Ufunuo 14:12). Hii humpatia mpokeaji imani ya kweli moyoni - amani na
Mungu.
Wapendwa, Shetani anachocheza nacho maishani mwetu ni imani zetu. Maana hutuletea udhaifu
wetu na dhambi zetu tulizozitenda mbele yetu na kutushawishi kuwa Mungu hawezi kabisa
kumkubali mtu mwovu. Hivyo unafuata ushauri wake mwingine kuwa, bora uendelee tu na maisha
hayo ya dhambi, na hivyo Mungu anadumu kuwa adui yetu. Na kama Shetani atashindwa kutufanya
tusimwamini kuwa Mungu atatupokea wadhambi, ataleta fundisho jingine, nalo ni la kujitahidi
kuokolewa kwa matendo ya sheria. Anasema Mungu hafanyi kila kitu, sasa kazana kwa matendo
matakatifu ili Mungu akupe maksi na uwe mshindi. Sasa tahadhari ni hii, katika hili la pili anafaulu
sana, maana inaonekana kana kwamba ni ukweli, naye anakuja kama malaika wa nuru (soma 2
Korintho 11:13-15). Lakini kumbuka neno la Mungu linasema, “kwa sababu hakuna mwenye mwili
atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria ----” (Warumi 3:20. Soma pia Wagalatia
2:16). Shetani akiishafaulu kuyumbisha imani yetu, matunda tutakayozaa daima yatakuwa najisi,
yasiyokubalika mbele za Mungu, yamechafuliwa na ubinafsi.
Lakini jambo tunalopaswa kufahamu ni kuwa imani sio swala lililo na mpaka kwamba watu wa kundi
fulani au dhehebu fulani ndio wenye imani ya kweli au imani bandia, hili ni swala la moyo wa mtu
kuhusu kile anachoruhusu akipokee.
Nataka niweke neno hili wazi kwamba msingi wa mafundisho ya imani zote duniani - zile za
madhehebu mengine na dini nyingine ni haki kwa matendo ya sheria. Ni msingi wa mafundisho ya
neno la Mungu kama lilivyofunuliwa kwa kanisa lake la Masalio (soma Ufunuo 12:17) ndiyo
unaofunua ukweli wa haki kwa imani. Lakini jambo moja la kusikitisha ni kuwa, mafundisho au
ukweli huu umechafuliwa na Shetani, na sasa wengi sana tunafahamu kuwa wokovu wetu
unategemea matendo yetu ya sheria. Mafundisho mengi tunayotoa yemejengwa katika mtazamo huo,
na ndio maana tumekuwa watumwa wa haki hii – binafsi - ambayo tunagundua kwamba ni mzigo
mkubwa, tusioweza kubeba. Kumbuka maneno ya Bwana Yesu katika Mathayo 23:4, “Wao hufunga
mizigo mizito na kuwatwika watu mabegaani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.”
Sasa kwa sababu ya kuwa na mafundisho hayo bandia, wengi sana wamejitenga na Mungu mioyoni.
Lakini, kwa upendo, anataka kuondoa mafundisho hayo potofu, na njia pekee anayoitumia ni haki ya
Kristo ambayo ni haki ya Mungu ipatikanayo kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Kila mmoja
wetu na afanye uamuzi kuchagua ni upande gani atakayosimama.
Wako wengi ambao hawatakubali kuifukuza haki yao binafsi iliyo ya sheria ili kuipokea haki ya
Kristo kwa imani; watajitenga na Kanisa la Mungu kabisa na kuwa maadui wakuu wa ile kweli ya
Kristo Yesu.
15
Tunapohitimisha sehemu hii inayohusu imani, hebu tukumbuke na kufahamu kwamba “Imani ni
kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” Kuamini ni
kujisalimisha kwa Mungu kulingana na alivyojifunua katika neno lake (Upendo). Maana roho
Mtakatifu huanzisha imani ndani yetu kwa njia ya neno la Mungu - Injili - (soma Warumi 10:17).
Mpendwa mwombaji, hebu tutafakari kwa makini ujumbe huu tunaoendelea kujifunza. Hebu
tutathmini imani zetu kwa nuru ya neno la Mungu ili isije kuwa tunapiga mbio bure (soma 1 Korintho
9:26, 2 Kor. 13:5).
Comments
Post a Comment