MAMBO YA KUFANYA/KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA UCHUMBA.
Katika kitabu cha Muhubiri 3:1 Biblia inasema “Kwa kila
jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Hivyo
mwanadamu katika maisha yake hapa chini ya jua kuna vipindi mbalimbali
anavyovipitia hii ni pamoja na kipindi cha uchumba kwa sehemu kubwa ya
watu.
Katika kipindi hiki yapo mambo mengi ambayo wachumba hufanya, mengine ni mazuri
na mengine hayafai kabisa. Na hii yote inatokana hasa na mitazamo au tafsiri ya
uchumba kwa watu husika. Fahamu kwamba tafsiri unayokuwa nayo juu ya mchumba
wako ndiyo inayokuongoza kujenga mahusiano ya aina fulani pamoja naye.
Lengo la somo hili ni;
Kuongeza ufahamu wa wachumba kuhusu kipindi hiki na Kuwapa vijana maarifa ya
kuwasaidia kuishi kwa nidhamu ya Ki-Mungu katika uchumba wao. Pia ni
kuwafikirisha vijana wanaotarajia kupita katika kipindi hiki mambo ya
kuzingatia. Si wachumba wengi wanajua, Mungu anawataka wafanye nini katika
uchumba wao au kwa lugha nyingine si wachumba wote wanaojua kwa nini kipindi
cha uchumba kipo. Naam katika somo hili tumeandika mambo hayo kinaga ubaga.
Kwa kuwa suala la uchumba ni pana na lina mitazamo mingi, yafuatayo ni mambo
tuliyozingatia katika uandishi wa somo hili;
- Kuna
makundi mbalimbali ambayo yana taratibu zao kuhusu mchakato wa mtu kumpata
mke au mume kikiwepo kipindi cha uchumba. Makundi hayo ni pamoja na
makanisa, makabila, familia nk.
- Wachumba
wanaweza kutofautiana kwa kiwango cha elimu, uchumi, ufahamu juu ya mambo
mbalimbali, kikabila, umri na hata kwa rangi pia.
- Kuna
baadhi ya wachumba hadi kufikia muda wanakubaliana kwamba watakuja kuishi
pamoja walishafahamiana tangu zamani na wengine hawakufahamiana.
- Wachumba
wanaweza wakatoka katika madhehebu/makanisa tofauti na hili ni kwa kuzingatia
madhehebu/makanisa mengi yaliyopo.
Lengo letu ni kuandika juu ya mwongozo wa Neno la
Mungu katika kipindi cha uchumba. kwa lugha nyingine, je Mungu anataka wachumba
wafanye nini katika kipindi chao cha uchumba?. Kumbuka uchumba ni
kipindi/wakati. Basi kama ni wakati jua kabisa kuna baadhi ya mambo ambayo ni
lazima yafanyike, kwani Biblia inasema katika Mhubiri 8:5b “ Na moyo wa
mwenye hekima hujua wakati na hukumu”, neno hukumu linamaanisha maamuzi,
mambo ya kufanya.
Yafuatayo ni mambo ya msingi kufanya katika kipindi cha uchumba;
Jambo la kwanza – Mruhusu Roho Mtakatifu
afanyike Bwana wa uchumba wenu
2Wakorinto 3:17 ‘Basi Bwana’ ndiye Roho; na alipo Roho wa Bwana, hapo
ndipo penye uhuru’.
Kumbuka Roho Mtakatifu ni msaidizi. Hivyo basi ni vema kumtumia vema hasa
katika nyanja hii ya mahusiano katika kipindi hiki cha uchumba. Ni Roho
Mtakatifu pekee mwenye uwezo wa kukujulisha mambo na siri nyingi kuhusu mchumba
wako hata kama yeye hataki kukueleza. Ukimruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana,
yeye atakuongoza katIka kufanya maombi yanayolenga maeneo ya msingi juu ya huyo
mwenzako. Kila mtu ameumbwa pamoja na mapungufu fulani au kwa lugha nyingine
mapungufu/ udhaifu (weakness) ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Roho Mtakatifu
anapokuwa Bwana wa mahusiano yako yeye atakusaidia kuona madhaifu au mapungufu
ya mwenzako kama kitu cha wewe kujivunia(Strength) kwa maana ya kuona udhaifu
wa mwenzako kama kitu chema na si kibaya.
Kumbuka Paulo katika 2Wakorinto 12:9-10. —‘Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa
furaha nyingi, ….kwa hiyo napendezwa na udhaifu——- maana niwapo dhaifu ndipo
nilipo na nguvu. Hivyo Roho Mtakatifu atabadilisha tafsiri ndani yako za vyote
unavyoona kwa mwenzako huenda juu ya umbile lake, umri wake, macho yake, kabila
lake viwe vitu vya wewe kujivunia. Zaidi Roho Mtakatifu pia atakuongoza katika
maombi yatakayosidia kuuondoa ule udhaifu ambao umekuja si katika mapenzi ya
Mungu, yaani wa kishetani.
Jambo la pili – ni wakati wa kuweka msingi
imara wa uchumba wenu na kufahamiana zaidi.
Hili jambo ni la muhimu kuzingatia. Ni vema wachumba wakatafsiri na
kuelewa vizuri maana ya uchumba. Wachumba wanapaswa kuwa na mipaka fulani
katika uchumba wao na kuwa makini kwa kujilinda na mazingira ya kila
namna ambayo yanaweza yakapelekea wao kuanguka dhambini. Ni vema mkajua kwamba
ninyi ni wachumba na si wanandoa. Na kama ni wachumba basi uchumba una mipaka
yake na hamruhusiwi kufanya mambo ya wanandoa. Mipaka hii iwe kwa habari ya
kutembeleana,kupeana zawadi, mawasiliano (ingawa mnapaswa kuwa makini na lugha
mnazotumia pia) nk. Lengo la kutafsiri misingi ya mahusiano yenu ni
kujiwekea mipaka na mazingira yatakayowasaidia kuishi maisha ya nidhamu,
ushuhuda na kumletea Mungu utukufu.
Sambamba na hili sehemu kubwa ya wachumba huwa wanakuwa hawafamiani vizuri.
Japo wapo baadhi ambao walianza tangu shule za msingi/sekondari/chuo na sasa
wamechumbiana hivyo kwa sehemu wanafahamiana vema. Kwa wale wasiofahamiana vema
huu ni wakati wa kumjua mwenzako vizuri kwa maana ya kabila lake, familia
yake, umri wake, interest zake, matatizo aliyo nayo yeye binafsi au ya
kifamilia, mitazamo yake juu ya mambo mbalimbali kama uchumba, ndoa, maisha,
wokovu, neno la Mungu nk. Huu ni wakati wa kumjua mwenzako kwa njia ya maswali
mbalimbali ya msingi yanayohusu vitu nilivyovitaja hapo juu. Lengo hapa ni
kujua mapungufu/madhaifu(weakness) na mazuri(Strength) za mwenzako ili mjue
namna ya kukabilana na mapungufu na namna ya kuendeleza yaliyo mazuri.
Ni vema pia kuulizana historia zenu za maisha ya nyuma. Kabla ya kuokoka
umepitia katika mifumo gani ya maisha ambayo imechangia kukufanya uwe ulivyo.
Kabla ya kumpata uliye mpata ulikuwa umefuatwa na wangapi na uliwakubalia au
la, na kama uliwakubali kwa nini mliachana, na sasa wako wapi, je bado
wanakufuatilia. Hii itawasaidia sana kujipanga vizuri kimaombi na katika
mahusiano yenu na zaidi itawasaidia kuweza kuchukuliana na kuhifadhiana katika
madhaifu ya kila mmoja.
Mungu anapowaunganisha anakuwa na kusudi maalum. Hivyo jua kwamba huyo mwenzi
uliyepewa umepewa kwa ajili ya kusudi fulani la Mungu. Ni wachumba wachache
sana ambao pindi wanapokutana kila mmoja anakuwa anajua walau kwa sehemu kwa
nini aliumbwa. Sasa ni vema mkae chini mfikiri, nini Mungu anataka kukifanya
duniani kupitia ninyi? Na zaidi angalieni kazi zenu au yale mnayoyasomea, Je
mtawezaje kuliimarisha agano la Bwana kwa pamoja kama mke na mume?.
Hapa maana yetu mnatakiwa kujibu maswali yafuatayo? Je ni kwa nini mlizaliwa?
Je kwa nini Mungu amekuunganisha na huyo uliye naye sasa? Na je kupitia elimu,
bisahara zenu au kazi mlizonazo mtawezaje kuimarisha agano la Bwana?, Kwa
kuzingatia vipawa na uwezo Mungu aliowapa, je ni wapi Mungu anataka kuwapeleka
na kuwafikisha? Kama ndani yenu mna huduma fulani, je ni watu gani ambao Mungu
atataka mshirikiane nao katika huduma hiyo?, je ipi ni nafasi yenu katika mwili
wa Kristo na taifa kwa ujumla? Ni vema zaidi mwanaume akajua wito/ kusudi
aliloitiwa ili pia amshirikishe na mwenzake.
Kufanikiwa kwa hili kunahitaji uwepo muda wa kutosha wa wachumba kukutana ili
kupanga na kuweka mambo yao mbalimbali, na kama ni watu walioko mbali basi
suala la mawasiliano kwa njia mbalimbali kama simu, barua pepe, na barua na
hata zawadi ni la muhimu.
Jambo la tatu- ni wakati wa kulinda wazo la Mungu hadi litimie.
Siku zote uamuzi wowote unaoufanya una gharama. Naam uchumba pia una gharama
nyingi Sana za kuzikabili kuliko unavyofikiri. Gharama hizo ni pamoja na muda,
pesa, mawasiliano, maombi, uhuru nk. Kumpata mchumba au mwenzi ambaye ni wa
kusudi la Mungu, usidhanie ndio umemaliza. Kama huo uchumba wenu ni wa mapenzi
ya Mungu muwe na hakika mtakutana na vita kubwa sana katika kipindi hicho cha
uchumba na lengo ni kuwatenganisha. Ni lazima mjifunze siku zote kuombeana kwa
kumaanisha maana Shetani naye yupo kazini ili kuvuruga hayo mahusiano.
Kumbuka huyo mwenzi ni agano toka kwa Bwana hivyo unawajibika kumlinda,
kumlinda ni pamoja na kuhakikisha wewe hausabibishi au haufanyiki chanzo cha
ninyi wawili kuanguka dhambini, au ukamwacha na kumsababishia majeraha ya
nafsini na hivyo kuharibu mahusiano yake na Mungu. Wapo watu waliofikia
kuharibu mahusiano yao na Mungu kisa mchumba, saa ya ibada imefika mchumba
anasema twende zetu out bwana, unataka kufanya maombi ya kufunga mchumba
anasema kesho nitakutoa out, inagharimu sana muda wa kuwaza pia kwa ajili yake
na familia yake au mahitaji mbalimbali aliyo nayo.
Zaidi pia uchumba unaweza kukunyima uhuru hata wa kuwa na maongezi na rafiki
zako, maana kuna baadhi ya watu huwa hawataki kuona mchumba wake anaongea au
kucheka na watu wengine, na pia kuna wengine ni wachumba lakini wamewekeana
taratibu ngumu utafikiri wanandoa kabisa na ukweli zinawatesa ila kwa sababu
hataki kumpoteza huyo mchumba wake inabidi avumilie. Jambo tunalosisitiza
hapa ni kwamba, uchumba una gharama nyingi angalia mahusiano yako na Mungu
yasiharibikie hapa.
Jambo la nne- ni wakati wa kupanga malengo na mikakati yenu ya
baadae.
Mithali 29:18a “Pasipo maono, watu huacha kujizuia’
Hili si jambo ambalo vijana wengi hulipa kipaumbele linavyostahili. Katika hili
ni vema wachumba wafikirie mapema ni aina gani ya maisha ambayo wangependa kuwa
nayo, na pia je ni aina gani ya ndoa wanataka kufunga, tatu je ni wapi
wangependa kuja kuishi kwa maishayaoyote. Haya yatawasaidia wahusika kujipanga
ndani na nje kukabiliana na yaliyo mbeleyao.Kamawanataka kufunga harusi
kanisani basi maana yake wanahitaji kuwa na maandalizi mazuri kifedha, waweke
katika muda kila wanalotaka kuelekea katika harusiyaoili iwasaidie kujiaadaa
mapema. Malengo yoyote yale ambayo mtaweka basi hakikisheni yanatekelezeka,
yanafikika, yanapimika na mnayapangia muda wa utekelezaji.
Mambo zaidi ya kuzingatia katika malengo yenu;
Katika hili ni vizuri wachumba waangalie nafasi yao kifedha imekaaje, na
changamoto zinazowakabili wote kwa pamoja. Je hali yao kifedha inawaruhusu
kuzikabili gharama za maandalizi ya ndoa kwa ujumla. Je hali ya kimaisha ya
kijana wa kiume inamruhusu wakati wowote baada ya kuchumbia aweze kufunga
harusi kama anataka. Je nafasi zao kielimu zikoje, je kama zinatofautiana ni
kwa kiwango gani? Na je tofauti zao kiuchumi na kitaaluma zinaweza kuwa kikwazo
kwao kuoana, au kwa wazazi wao nk. Na je baada ya kuwa wamegundua na kupima
uwezo wao katika hayo mambo mawili, je wanaweza wakasaidianaje ili wafike
mahali pazuri wote wawili.
Vijana wengi wa kiume huwa wanakosea sana hapa, wengi huwa wanasema sitaki
kuchumbia/kuoa mpaka niwe nimesha jikamilisha kiuchumi, niwe angalau na maisha
mazuri. Sisi hatushauri sana dhana hii, ukweli ni muhimu kwa kijana wa kiume
akjikamilisha kwa yale mambo ya msingi. Lakini fahamu kwamba kuna wakati
mwingine kuendelea kwako kiuchumi, au kuvuka kwako kimaisha ni rahisi zaidi
pale unapokuwa na mchumba au ndoa yako. Tunasisitiza tena ni vema wachumba
wakae chini na kufikiri ni kwa namna gani wataendelezana kiuchumi na kitaaluma.
Angalizo, ni vema uwe na uhakika kweli huyo mtu ni wa mapenzi ya Mungu kwa
maana ya kuwa ni wa kwako kweli, maana wapo wachumba ambao wamekuwa
wakisaidiana mpaka kulipiana ada, kupeana mitaji, kununuliana nyumba, magari
nk, halafu mwishowe mmoja anavunja maagano, maumivu yake ni makubwa sana.
Jambo la tano – ni wakati wa matengenezo na
kuzijenga nafsi zenu
Wachumba wengi huwa wanafichana mambo mengi sana wanapokuwa wachumba na matokeo
yake hawayashughulikii mapema na hivyo yanakuja kuwaletea shida kwenye ndoa.
Huenda kabla hujakubaliwa wewe tayari mwenzako alikuwa amesha wakubali vijana
au mabinti wengine kwamba ataolewa nao au kuwaoa. Pia kama ni msichana
huenda ameshawahi kubakwa, au kutokana na masumbufu ya kupata mtu sahihi na
wakati mwingine kuachika mara kwa mara imefika mahali huyo msichana akasema
sitaki kuja tena kuolewa. Zaidi huenda mmoja wenu huko nyuma
ameshawahi kufanya uasherati au zinaa kabla hamjachumbiana. Au kuna mwingine
amekuwa akisumbuliwa na tatizo la harufu, kufanya tendo la ndoa na mapepo nk.
Haya yote na mengine mengi yanayofanana na haya yana athari kubwa sana kiroho
na kimwili kwenu kama wachumba na wanandoa watarajiwa kama hayatashughulikiwa
vema katika kipindi hiki cha uchumba. Licha ya kuwa na athari mambo hayo
yamepelekea nafsi za watu au wachumba wengi kujeruhika. Nafsi inapojeruhiwa
inaharibu ndani ya mtu mfumo wa kufanya maamuzi, mfumo wa utiifu kwa Mungu
wake, mfumo wa kunia na kuhisi pia. Sasa mifumo hii inapoharibika inapelekea
watu kufanya maamuzi ambayo yapo nje ya mapenzi ya Mungu kabisa. Nawajua baadhi
yao ambao wameacha na wokovu, na, wengine wamekata tamaa ya kuolewa, wapo
walioamua kuolewa na mataifa ilimradi ameolewa nk.
Hivyo basi tumieni wakati huu kufanya matengenezo na kujengana nafsi zenu kwa
maana ya kuombeana sana, pili kwa kuongeza ufahamu wenu katika neno la
Kristo hasa maandiko yanayolenga uponyaji katika nafsi zenu, tatu kufuta na
kufisha mapatano/maagano yote ambayo mmoja wenu aliyafanya huko nyuma na watu
wengine na pia kufuta picha za kubakwa na kujenga ufahamu wa mtu aliyeathirika
kisaikolojia kutokana na mambo kama hayo kwa njia ya Damu ya Yesu. Hatua hizi
zitawasaidia kurejesha mifumo iliyoharibika na kuziruhusu nafsi zenu zifanye
kazi kama inavyotakiwa.
Jambo la sita – ni wakati wa kujua taratibu
mbalimbali kuelekea kwenye ndoa
Tumeshasema, kila dhehebu au kabila wana taratibu zao kuhusu
uchumba hadi ndoa. Hivyo ni vema wachumba, wakafuata taratibu ambazo zimewekwa
na makanisa yao hasa zile ambazo zipo katika mapenzi ya Mungu. Lakini pia
lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya taratibu za makanisa, makabila na hata
madhehebu ambazo nyingine zipo tu lakini hazitekelezeki na nyingine
hazimpendezi Mungu.
Sasa ni vema wachumba wazijue hizo taratibu na wajue je wanaweza kuzitekeleza
au la, na kama hawawezi wafikirie kabisa wanafanyeje. Mfano kuna baadhi ya
makanisa ambayo hayaruhusu mtu wa kwao aoe au kuolewa na mtu wa nje ya dhehebu
hilo. Sasa hii ina maana kama una mchumba wa aina hiyo jipange kujibu maswali
ya wazee wa kanisa na Mchungaji vizuri. Na zaidi kuna baadhi ya makabila na familia
hazitaki uoe au kuolewa na watu nje ya kabila lako, au aliyekuzidi umri kama
wewe ni kijana wa kiume nk. Hivyo ni vema kuzijua hizo taratibu ili mjue
mnajipangaje kukabiliana nazo. Ushauri wetu ni huu kama una uhakika huyo mtu ni
wa kutoka kwa Mungu basi simamia la Bwana maana lipi jema, kumpendeza Mungu au
wanadamu?. Kumbuka Mungu ndiye mwenye ratiba ya kila mmoja wetu.
Suala la kukagua/kupima afya zenu kwa pamoja.
Kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa suala la ukimwi limechukua sura mpya na
kuleta mtafaruku ndani ya kanisa hasa kwa vijana wanochumbia kabla ya kupima
afya zao. Siku hizi jambo hili limewafanya wachungaji kuomba sana kwa habari ya
vijana ndani ya kanisa. Sasa kama mlikuwa hamjapima afya zenu mpaka
mmechumbiana basi chukueni hatua mwende kupima. Ni vema wachumba wakapima
mapema afya zao ili jambo hili lisije likawaletea shida baadaye, maana kwa
sheria ya nchi yetu wachungaji hawaruhusiwi kufungisha ndoa kama mmoja wa
wahusika ameathirika.
Upimaji wa afya zenu ni wa muhimu kwani, ndani ya makanisa kuna rekodi ya
vijana wengi tu ambao wameshaathirika na huenda si kwa sababu ya zinaa, maana
kwa mujibu wa watu wa afya njia za maambukizi ni nyingi. Kuna wengine
wamezaliwa nao, kwa nia ya kuongezewa damu,kutumia vifaa kama nyembe, sindano
nk. Hata hivyo swali la msingi inabaki kwamba je, liko tumaini kwa mtu
aliyeathirika kuoa au kuolewa?
Tukueleze hivi, hakuna jambo gumu lolote la kumshinda Bwana, hii ni pamoja na
ukimwi, kama Mungu alimfufua Lazaro, alitenganisha bahari ya Shamu na watu
wakapita, kama Yesu alitembea juu ya maji, basi naomba ujue kwamba
Ukimwi hauwezi kuzuia kusudi la Mungu hapa duniani kwa wale awapendao na
kwa sababu hiyo tunasema hata kama mtu ana ukimwi na Mungu bado ana kazi naye
hapa duniani, hakika atamponya huo ukimwi na atampa mke au mme.
Faida na lengo la kupima ni hili, hata kama majibu yatatoka mmoja ameathirika
isiwe mwanzo wa ninyi kuachana. Kama mna uhakika Mungu aliwaanganisha huu ndio
wakati wa kurudi mbele za Mungu kwa maombi ya uponyaji na kujipanga zaidi juu
ya hilo.
Jambo la saba – ni wakati wa kuongeza ufahamu wenu kuhusu nafasi
yako kwenye ndoa.
Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu anakupa mke au mme? Yamkini zipo
sababu nyingi lakini baadhi yake ni; Mungu anakupa mke kama msaidizi, mlinzi,
na pia unapopata mke au mme unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana na pia ni kwa
sababu ya zinaa ndio maana unahitaji mwenzi. Hizi ni baadhi ya sababu zilizoko
ndani ya Biblia. Hivyo basi tafuteni wanandoa mnaowaamini na zaidi
waliokoka muwaulize kuhusu wajibu wa kila mmoja kwa
nafasi yake kwenye ndoa. Katika hili baadhi ya makanisa huwa yana
utaratibu wake wa nani atahusika na maelekezo ya aina hii kwa wachumba. Hivyo
kama kanisa lako lina utaratibu huo, fuata huo utaratibu.
Katika ndoa kuna mambo mengi sana ambayo mtatakiwa kufanya, ni vema kufuata
mwongozo na ushauri wa viongozi wenu au wachungaji wenu kuhusu nini mnatakiwa
kufanya katika ndoa yenu. Angalizo hapa ni hili, uwe makini na vyanzo vya
ushauri au mafunzo katika eneo hili ili lisije kuleta madhara baadae. Usitafute
wala kufuata kila ushauri, bali sikiliza pia uongozi wa Mungu ndani yako.
Jambo la nane– Msifanye tendo la ndoa, maana jambo hili litaharibu
mpango wa Mungu na kusudi lake kupitia ninyi.
Wakati wa uchumba, si wa kufanya mapenzi au kufanya michezo ya mapenzi.
Tunarudia tena ili kuonyesha msisitizo kwamba chonde chonde jamani, uchumba sio
ndoa, maana uchumba unaweza kuvunjika. Hairusiwi kabisa kwa wachumba kufanya
mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa kabla ya ndoa. Kitendo cha Mungu
kukujulisha/kukupa huyo mwenzako kama mke/mume mtarajiwa haina maana mna haki
ya kufanya mambo ya wanandoa. Mungu kukupa huyo mwenzako sasa ni taarifa
kwamba huyu ndugu ndiyo atakuwa mkeo au mmeo na anakupa taarifa sasa ili
ujipange kufanya mambo ya msingi mnayotakiwa kuyafanya katika kipindi cha
uchumba. Kipindi cha uchumba ndicho kipindi ambacho wachumba wengi sana
wanavuruga kusudi la Mungu, na kuharibu maisha yao ya baadae na ndoa yao kwa
ujumla.
Ndoa nyingi sasa hivi zina migogoro kwa sababu wakati wa uchumba walidiriki
kufanya tendo la ndoa. Vijana wengi hawajajua kufanya tendo la ndoa kipindi cha
uchumba lina madhara gani kwao na ndio maana wengine wanafanya. Biblia inasema
katika Mithali 6:32 “Aziniye na mwanamke hana akili kabisa, afanya
jambo litakalomwangamiza nafsi yake mwenyewe”. Hata kama ukifanya tendo la
ndoa na mchumba wako ambaye mlibakiza siku moja kufunga harusi, bado umezini.
Ndani ya nafsi ya mtu kuna akili, hisia, nia na maamuzi. Biblia inaposema
afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake ana maana hii, dhambi hii
inapofanywa, ina haribu mfumo wa utiifu na uamnifu kwa Mungu wako, inapelekea
kukosa usikivu wa rohoni kabisa, ina haribu mfumo wa kufikiri, kunia na kufanya
maamuzi. Na kwa sababu hiyo si rahisi tena kusikia na kutii uongozi wa Roho
Mtakatifu. Kwa watu ambao wamezoea kuwa na mahusiano mazuri na Mungu
watanielewa ninachosema hapa.
Zaidi kuna baadhi ya wachumba kweli hawafanyi tendo la ndoa bali wanafanya
michezo ya mapenzi. Michezo ya mapenzi (Fore play) ni maalum kwa ajili ya
wanandoa, na ni sehemu ya tendo la ndoa. Hivyo kufanya michezo ya mapenzi ni
kufanya mapenzi kwa sababu ile ni sehemu ya mapenzi. Kuna vitu
unavichochea, unaamusha hamu ya mapenzi au unayachochea mapenzi. Biblia
inasema katika Mhubiri 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na
kwa ayala wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata
yatakapoona vema yenyewe.”
Mungu pia anachukia michezo ya mapenzi soma Isaya 57:4-5 “Mnafanya
dhihaka yenu juu ya nani, juu ya nani mmepanua vinywa vyenu, Na kutoa ndimi
zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati
ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi….. Wachumba wengi
hawajui haya kwa sababu si makanisa yote yanayofundisha maswala ya mahusiano ya
wachumba kimpana.
Mpaka hapa tunaamini umeshajua hasara za jambo hili na utazijizuia kabisa
kulifanya. Michezo ya mapenzi ni pamoja na kunyonyana ndimi, kushikana sehemu
ambazo zinaamsha ashiki ya mapenzi kama sehemu za siri, matiti, kiuno nk,
pamoja na kuangalia picha za ngono. Katika kipindi ambacho tumemtumikia Mungu
kupitia vijana tumejifunza na kukutana na kesi mbalimbali za aina hii na kuona
namna Shetani anavyovuruga mpango wa Mungu kwa vijana. Mwenye sikio na asikie
neno ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa.
Ni imani yetu kwamba mambo haya nane yameongeza ufahamu na hivyo kuwa maarifa ya kutosha kukusaidia kuenenda kwa mapenzi ya Mungu katika kipindi cha uchumba.
Comments
Post a Comment