WITO WA WOKOVU KWA ULIMWENGU

 



Katika kitabu cha Warumi 13:12 tunasoma, “Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia -----.”
1 Petro 4:7 inasema, “lakini mwisho wa mambo yote umekaribia, basi iweni na akili, mkeshe katika
sala”. Mwisho wa mambo yote! Mwisho wa biashara, elimu, kazi, vyeo, kilimo, anasa, mwisho wa
dunia na vyote vilivyomo. Lakini mbona mwisho huu haujafika?
2 Petro3:9 inasema, “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake---- bali huvumilia kwenu, maana hapendi
mtu yeyote apotee bali wote wafikilie toba.”
Malaika wa Kwanza
Ufunuo 14:6-7, “kisha nikaona malaika mwingine akiruka katikati ya mbingu, mwenye injili ya
milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,
akasema kwa sauti kuu, mcheni Mungu na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu
yake imekuja, msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemichemi
za maji”.
ß Malaika ni nani? Ni watumishi wa Mungu (soma Waebrania 1:7, Ufunuo 19:10). Hivyo malaika
hawa huwakilisha watumishi wa Mungu (wanadamu) wanaotangaza ujumbe huo. Sasa hebu tutafakari
ujumbe au wito wa Mungu kwa njia ya malaika huyu wa kwanza. Malaika anasema:
• “Mcheni Mungu.” - Kumcha ni kumpa mhusika heshima iliyo ya juu sana. Hivyo Mungu
anatuita tumpe yeye heshima iliyo kuu sana na kumpa nafasi ya kwanza katika maisha yetu
badala ya kutanguliza nafsi ambazo hutufanya tuwe na Miungu mingine (soma Kutoka 20:3).
Tutii amri zake.
• “Na Kumtukuza.” - Tumpe Mungu utukufu wake. Njia ambayo kwayo tutampa utukufu ni kwa
kuishi maisha matakatifu ya utii kamili kwa amri za Mungu. Ni kuacha dhambi na kuishi maisha
ya ushindi katika Kristo Yesu (soma Mathayo 5:16, Waefeso 5:8-10, Yohana 15:8). Haki kwa
imani.

• “Kwa maana saa ya hukumu yake imekuja.” - Saa ya hukumu ni ule wakati au kipindi cha
huduma ya Yesu katika chumba cha Patakatifu pa Patakatifu mbinguni; huduma ambayo
iliwakilishwa na huduma ya siku ya upatanisho katika nyakati za huduma ya Patakatifu pa
duniani kama tulivyojifunza katika somo lililohusu Patakatifu. Hukumu ni kuamua kuwa mtu
huyu hana hatia hivyo yuko huru au kuwa ana hatia hivyo aadhibiwe. Kama tulivyoona, sasa
tunaishi katika saa hiyo ya hukumu, katika siku kuu ya upatanisho (soma Danieli 8:14, 7:9,10,13,
1 Petro 4:17). Wale wanaomuamini Yesu wanahesabiwa haki na kukubaliwa kwa ufalme wa
Mungu - Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima. Wale wasioamini wanaandikwa
katika kitabu cha hukumu (soma Ufunuo 3:5, 20:12). Saa hiyo ni sasa.
• “Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemichemi za maji.” Hapa neno la
Mungu linatukumbusha kuhusu ibada (msujudieni) na pia linatueleza ni kwa nini tumsujudie,
linasema kwa kuwa ni Muumbaji. Unajua jambo pekee linalomtofautisha Mungu wa kweli na
miungu mingine ya uongo ni uwezo wake wa uumbaji. Katika ibada ya dini nyingi duniani, watu
wamekuwa wakiabudu vitu vingine badala ya Mungu wa kweli, huku wakidhani wanamwabudu
Mungu Muumbaji. Je, unawezaje kujua kama unamwabudu Mungu wa kweli aliyeumba mbingu
na nchi na bahari na vyote vilivyomo? Je, kuna ishara yoyote inayotajwa katika Biblia kuonyesha
jambo hilo? Ndiyo, hebu tusome. Kutoka 31.13, “Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni
ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi
Bwana niwatakasaye ninyi.” Ezekieli 20:12, “Tena naliwapa Sabato zangu, ziwe ishara kati ya
mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndiye niwatakasaye.” Ezekieli 20:20,
“Zitakaseni Sabato zangu, nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi
ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Ishara hii inatuelekeza moja kwa moja katika amri ya nne kati ya zile amri kumi za Mungu. Hii
ni amri ambayo watu wengi sana duniani hawaishiki, tena watu wa dini zote, wakati hiyo ndiyo
ishara pekee ya kumwabudu Mungu wa kweli. Hii inaonyesha jinsi watu wengi wamekuwa
wanaabudu miungu mingine badala ya Muumbaji. Lakini je amri hiyo ya nne inasemaje? Kutoka
20:8-11 inasema, “Ikumbuke siku ya sabato uitakase, siku sita fanya kazi, utende mambo yako
yote, lakini siku ya Saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote,
wewe, wala mwana wako, wala binti yao. Wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala
mnyama wako wa kufuga. Wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita
Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba, kwa
hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato, akaitakasa.” Soma pia Mwanzo 2:1-3.
• Neno la Mungu halituambii kuwa tuchague siku yoyote katika wiki ili iwe Sabato. Linasema si
yetu, ni ya Bwana. Siku aliyostarehe akaibariki na kuitakasa. Siku nyingine sita hazina utakaso
wala mibaraka ya Sabato, hivyo haziwezi kuwa siku ya Sabato. Siku ya saba ya juma (wiki)
ndiyo Sababo, na siku hiyo ni Jumamosi. Kumbuka msomaji, jambo lolote lililo kinyume na
neno la Mungu ni nia ya mwili (nafsi), ambayo ni uadui juu ya Mungu, ambao ndio dhambi.
Angalia ibada yako isiwe ya bure (somo Mathayo 15:8-9). Hivyo wote wanaotaka Mungu
muumbaji awe Mungu wao wanapaswa kuonyesha ibada yao ya kweli kwa kuitunza Sabato na
wala si vinginevyo. Wote watakaokataa ishara hii ya Sabato watakuwa wanasujudia kitu
kingine. Sabato inamtofautisha na kumtangaza Mungu kama muumbaji.
• Lakini malaika huyu, pia ana injili ya milele. Injili ya milele ndizo habari njema za wokovu
katika Kristo Yesu ambazo umekuwa ukizisoma katika maelezo yaliyopita. “Wala hakuna
wokovu katika mwingine awaye yote, maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa
wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” isipokuwa la Yesu (Matendo 4:12).
• Huu ndio ujumbe ambao unatakiwa uhubiriwe kwa watu wa mataifa yote kuwa Yesu ni
mwokozi pekee wa ulimwengu na wale wanaomwamini wataonyesha imani yao kwa kuzishika
amri zake ikiwemo na Sabato ya siku ya saba ya juma, yaani Jumamosi.
Malaika wa Pili
Ufunuo 14:8, “Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, umeanguka, umeanguka
Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya
uasherati wake.”
• “Umeanguka.” - Neno hili limetumika kuonyesha hali ya kuuacha ukweli wa neno la Mungu
kama msingi pekee wa imani na kugeukia mafundisho mengine yasiyo na msingi katika
maandiko (soma Mathayo 7:24-27). Hili ni anguko la Kiroho. Anguko hili limeelezwa katika
ujumbe huu wa malaika wa pili kama matokeo halisi na yasiyoepukika kwa mtu yeyote au dini
yoyote isiyokubali kuupokea ujumbe wa malaika wa kwanza. Kumbuka malaika wa kwanza
anahubiri injili ya milele (yaani wokovu katika Kristo Yesu pekee). Anatuita tumtukuze Mungu
kwa kuzishika amri zake. Anatuita tumpe Mungu heshima ya juu sana na nafasi ya kwanza katika
maisha yetu, kumsujudia (kumwabudu) na kuonyesha ibada hiyo ya kweli kwa kuitunza na
kuitakasa Sabato ya siku ya saba ya juma kumtukuza Mungu kama muumbaji wa mbingu na nchi
na bahari na vyote vilivyomo. Huu ndio mpango wa Mungu.
Kwa hiyo kuukataa (kutokuupokea) ujumbe huo wa malaika wa kwanza, ni kuukataa mpango
halisi wa Mungu na kuanguka kiroho. Na popote neno la Mungu linapokataliwa, Shetani
huingiza mafundisho ya uongo ili kuchukua nafasi hiyo. Ndiyo maana mafundisho ya dini zote
tulizo nazo leo, yako kinyume kabisa na Mungu. Na ndio sababu ya kuwa na dini mbalimbali na
madhehebu mengi sana tofauti, huku tukidai tunamwamini na kumwabudu Mungu mmoja. Huu
ni uongo wa shetani ili kuwapoteza wanadamu (soma Mathayo 15:8-9, 2 Kor. 11:13-15).
Usalama wetu ni kukubali wito wa Mungu kwetu kama unavyoelezwa katika ujumbe wa malaika
wa kwanza.
• “Babeli, mji ule ulio Mkubwa.” - Kwa mara ya kwanza katika Biblia mji ulioitwa Babeli
ulijengwa na mtu aliyeitwa Nimrodi, ambaye alifanya vita kubwa sana dhidi ya Mungu kwa
kuwafundisha watu kwenda kinyume na neno la Mungu. Alianzisha ufalme wa kwanza kabisa
duniani uliokuwa kinyume na Mungu (soma Mwanzo 10:8-14). Miji hii mikubwa aliyoijenga
ndiko kulikuwa chimbuko la ibada nyingi za uongo tunazoziona leo. Hebu angalia jinsi Nimrodi
alivyopingana na Mungu. Katika kitabu cha Mwanzo 1:28 tunasoma, “Mungu akawabarikia,
Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi ----.” Na katika mwanzo 9:11 tunasoma,
“na agano langu nitalithibitisha nanyi, wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya
gharika, wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo kuiharibu nchi.” Huo ndio ulikuwa
mpango wa Mungu. Lakini chini ya Nimrodi watu walifanya mpango ulio kinyume,
“Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbunguni; tujifanyie jina,
ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote” (Mwanzo 11:14). Kwa hiyo wao hawakutaka
kutawanyika usono pa nchi, na pia hawakumwamini Mungu kuwa hataleta tena gharika, hivyo
wakaamua kujenga mnara na kilele kifike mbinguni, ili gharika ikija tena, wapande juu ya mnara
na kujiponya. Jambo jingine muhimu kulitambua ni ile kanuni iliyowasukuma kufanya hivyo.
Nafsi, nafsi, nafsi, ndiyo waliyoitii, badala ya kumtii Mungu, maana walisema tujijengee,
tujifanyie jina, tusipate…, - binafsi. Hii ndiyo iliyokuwa kanuni iliyomwongoza Shetani kuasi
(soma Isaya 14:13-14). “Nita” “mimi”; ndiyo msingi wa anguko la mwanadamu katika dhambi,
na ndio msingi wa imani au dini zote zisizojengwa katika neno la Mungu. Hiyo, ndiyo kanuni ya
Babeli. Sasa, mji ule uliojengwa na Nimrodi uliharibiwa lakini mji huo wa Babeli ukajengwa
tena na mfalme aliyeitwa Nabukadreza kwa kanuni ile ile ya kujitukuza nafsi kuliko Mungu
(soma Danieli 4:29-32). Mji huu ulikuwa mkubwa. Ukaitwa “mji wa dhahabu,” “utukufu wa
dunia nzima” na ufalme huo wa Babeli ulitukuka sana. Lakini kwa sababu ya kumwasi Mungu
na kutompa utukufu, mji huu nao uliharibiwa (soma Isaya 21:9, Yeramia 51:52-64). Hivyo mji
huu ya Babeli unawakilisha mifumo yote ya dini za uongo zilizomwasi Mungu. Na kama mji huu
halisi ulivyoanguka na kuangamia na hata leo haupo, inasimama kuwa ishara kwamba imani au
dini zote zisizojengwa katika Biblia mwisho wake ni kuanguka na kuangamia milele (soma
Ufunuo 18:5-24).
Ndugu msomaji, umesimama upande gani? Katika imani inayowakilishwa na Babeli, ambazo ni
imani zilizoanguka; au upande wa Bwana? Hii ni nafasi yako ya pekee sana kuchagua wokovu
kama unavyofunuliwa na neno la Mungu.
• “Maana --- uliwanywesha mataifa yote mvinyo--- ya uasherati wake.”
ß Kunywesha ni kufundisha (soma Yohana 4:14, 7:37-38).
ß Mvinyo ni mfano wa mafundisho ya uongo. Kama tunavyofahamu kuwa mvinyo ni
pombe au kileo, na mtu anapokunywa analewa na matokeo ya kulewa tunayafahamu.
Hivyo mfumo huu wa imani au dini au mafundisho ya uongo, ambayo yana
chimbuko lake katika mji wa Babeli, yameenea kwa mataifa yote na kusababisha
watu kulewa na mafundisho hayo hata wasitambue kweli ya neno la Mungu.
Yeremia 51:7 inasema, “Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa
Bwana. Kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu
hiyo mataifa wameingiwa wazimu.” Mambo ya kutisha ajabu. Kama mataifa
wamekuwa na wazimu kwa sababu ya mafundisho hayo ya uongo ya kidini, je,
tunaweza kushangaa ni kwa nini dunia yetu imejaa magomvi, mauaji, zinaa, ubakaji,
vita, dhuluma na kuharibika kwa maadili mengine mengi? Na katika hali hiyo
ukweli wa neno la Mungu unaposemwa wazi, watu hawa walio na wazimu
watawatesa na kuwaua watu wa Mungu.
ß Uasherati wake - huwakilisha uhusiano usio halali nje ya ndoa. Neno la Mungu
huelezea uhusiano kati yake na watu wake kwa mfano wa uhusiano wa ndoa -
Mungu kama mume na watu wake kama mke wake. Mambo haya ni ya kiroho na
tunatakiwa kuyatambua kwa jinsi ya rohoni (soma 1Kor. 2:13-15). Uhusiano huo
umeelezwa katika Yeremia 3:14, Isaya 54:5-6 na Waefeso 5:25-32. Kwa hiyo
tunapomwacha Mungu wetu kwa kutolishika neno lake, ijapokuwa tuwe na dini na
kuabudu, lakini tutakuwa tunaabudu Mungu mwingine asiye wa kweli, na hivyo
tutakuwa tunafanya uzinzi kiroho. Kwa hiyo Babeli ilimwasi Mungu na kufundisha
uongo ambao leo umeenea katika mataifa yote. Mafundisho mengi yaliyomo katika
baadhi ya madhehebu ya kikristo, Uislamu, Buddha, Hindu, dini za kimila nk. ni ya
uongo, na hivyo yanawakilisha Babeli (mke aliyemwasi mumewe) kiroho.
ß Sasa, kama miji ile ya Babeli iliishaanguka, je, leo bado tunaweza kusema kuna mji
wa Babeli? Ndiyo. Leo pia bado kuna Babeli ya sasa ambayo siyo mji bali ni
mamlaka ya dini ambayo ndani yake yamejaa mafundisho ya kipagani, na
mafundisho hayo yameenea katika dini mbali-mbali duniani. Hivyo badala ya
mamlaka hiyo ya kidini kuwa mke wa kristo, sasa inaitwa, “Babeli Mkuu, mama wa
makahaba na machukizo ya nchi” (soma Ufunuo 17:1-6). Lakini jina hili ni la siri,
unaweza tu kulitambua kutokana na nuru ya neno la Mungu. Na hiyo ndiyo mamlaka
ya kanisa la Rumi (Roman Catholic) kama mama, na makanisa mengine yote
yanayofuata mafundisho yake kama watoto wake ambao pia ni makahaba (soma
Ufunuo 17:18).
Ujumbe wa Malaika wa Tatu
Ufunuo 14:9-12, “Na mwingine, malaika wa tatu, akafuata, akisema kwa sauti kuu, mtu awaye yote
akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake au katika
mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo
kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake, naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya
malaika watakatifu, na mbele za mwanakondoo. Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele
na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na
kila aipokeaye chapa ya jina lake. Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za
Mungu na imani ya Yesu”.

Malaika huyu wa tatu anauonya ulimwengu juu ya kumsujudia mnyama na sanamu yake na kuipokea
chapa yake. Hukumu ya kutisha inatangazwa dhidi ya wote watakaomsujudia mnyama huyu -
kutupwa katika ziwa la moto - ni hukumu ya kutisha. Kwa nini usijiepushe na mnyama huyu? Je,
unamfahamu? Hebu tunapoelekea mwishoni, jifunze kumfahamu mnyama huyu.

- “Mnyama” – Biblia inatafsiri mnyama kuwa ni mfalme au ufalme (soma Danieli 7:15-17, 23-
25.) Katika Ufunuo 13:11-18 inaelezea kuhusu mnyama (ufalme) utakaoilazimisha dunia na
wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama anayeitwa wa kwanza na sanamu yake.
Mnyama huyu wa kwanza ni yule anayetajwa katika Ufunuo 13:1-8. Huyu ni yule aliyepokea
au kurithi mamlaka ya dola ya Kirumi (soma Ufunuo 13:1-2.) Joka ni tafsiri ya mamlaka
aliyotumia Shetani ili kumwangamiza Bwana Yesu (soma Ufunuo 12:1-5) na maandiko
yanaonyesha wazi kuwa mfalme wa Kirumi (Herode) alianzisha mauaji makuu ya watoto ili
ikiwezekana amwangamize Yesu, lakini Mungu alimwokoa na mauaji hayo (soma Mathayo
2:13-23.) Mnyama huyu, ambaye watu wote watalazimishwa kumsujudu na ambaye ni mrithi
wa kiti ch enzi cha dola ya Kirumi, si mwingine isipokuwa ni MAMLAKA YA KANISA LA
RUMI au UPAPA. Hivyo neno la Mungu linafunua jambo muhimu sana kwa kila mtu
aishiye duniani kwamba usalama wetu pekee, ili kuokoa roho zetu, ni kutomsujudia Mnyama
na sanamu yake. Jambo hili liko mbele yetu na kila mtu atatakiwa kufanya uchaguzi,
kwamba amsujudie Mungu aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vyote vilivyomo kwa
kuzishika amri zake (soma Ufunuo 14:6-7) au amsujudie mnyama na sanamu yake, ambako
kwa kweli ni kumsujudia Shetani mwenyewe (soma Ufunuo 13:2.) Katika Ufunuo 13:11-18
inaongezea juu ya ufalme (utawala) utakaolazimisha dunia na wote waliomo kumsujudia
Rumi lakini Ufunuo 17:12-18 inaongezea kufunua jambo hilo zaidi kwa kuonyesha kuwa
licha ya ufalme au utawala mmoja utakaolazimisha ibada hii iliyo kinyume na Mungu, tawala
zingine pia duniani (wafalme kumi) wataungana katika kutekeleza jambo hilo. Hivyo
tunachojifunza hapa ni kuwa tawala zote za dunia zitaungana kulazimisha ibada kwa kufuata
mwongozo wa Kanisa la Rumi (soma Ufunuo 16:13-14.) Wafalme hawa watapokea
mamlaka pamoja na yule mnyama, yaani kutakuwa na muungano maalum kati ya Kanisa la
Rumi na mataifa ya dunia hii kutimiza jambo hili. Kumbuka kuwa Rumi inamafundisho yake
yaliyo kinyume kabisa na neno la Mungu.

- “Sanamu ya Mnyama” – Sanamu ni mfano wa kitu halisi. Kama Mnyama ni mamlaka ya
Kanisa la Rumi (RC), sanamu yake ni mamlaka ipi? Mamlaka nyingine ya Kikristo iliyofuata
baadhi ya mafundisho ya Rumi na hivyo kuchanganya neno la Mungu na mapokeo, ni
Uprotestanti. Hivyo sanamu ya Mnyama ni UPROTESTANTI ULIOASI, ambao ijapokuwa
unadai umejitenga na Kanisa la Rumi, lakini mafundisho yao makuu ni yaleyale ya Rumi, na
leo makanisa hayo yako mbioni kurudi kwa mama yao – KUUNGANA (soma Ufunuo 17:5.)
- “Chapa Katika Kipaji cha Uso” – Akili ndiyo sehemu muhimu inayohusika katika ufahamu
na uamuzi mtu unaoweza kuufanya (soma 2 Wakorinto 5:13, Waefeso 5:15-17.) Hivyo,
kukubaliana na mafundisho na mfumo utakaowekwa na serikali za dunia zikishirikiana na
Kanisa la Rumi, ndiko kupokea chapa katika kipaji cha uso. Jambo la muhimu kukumbuka ni
kuwa kimsingi imani ya Kirumi inayakubali mambo yote ya msingi yaliyomo katika dini
nyingine, na hivyo kwa msingi huo, hata dini nyingine zitakubaliana na mpango huu. (Je, hii
ni kweli?)
- “Chapa Mkononi” – Mikono yetu ndiyo viungo vikuu vya utendaji, kwa maana ya kutekeleza
kazi. Ijapokuwa mwili mzima unahusishwa katika kazi, lakini mikono yetu ndio hasa hufanya
sehemu kubwa kivitendo. Hivyo kupokea chapa ya Mnyama katika mkono ni kutekeleza
kivitendo maamuzi au maelekezo yatakayotutaka tumsujudie Mnyama kwa kuiheshimu
Jumapili kama siku ya Bwana.

Katika Ufunuo 13:8 inasema, “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake
halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya
dunia.” Maandiko yako wazi kuwa wale ambao hawatamsujudu Mnyama ni wale ambao majina yao
yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo. Lakini je, ishara ya kuonyesha kuwa mtu
anamsujudu Mnyama (Rumi) itakuwa nini? Ishara ya alama hiyo ni kuiheshimu Jumapili kama siku
ya Bwana. Tulitangulia kujifunza kuwa Mungu Muumbaji anasema Sabato ndiyo ishara kati yake na
watu wake ya kuwa yeye ndiye Mungu wao (soma Ezekieli 20:12,20) na Sabato ni Jumamosi.
Lakini kwa sababu yule Mnyama alipokea mamlaka toka kwa joka ambaye ni Shetani na ambaye
ameendelea kupingana na Mungu tangu alipoasi, yeye naye aliweka siku inayoonyesha kuwa na yeye
(Shetani) anaabudiwa au kusujudiwa, na siku hiyo ndiyo Jumapili (soma Mathayo 15:8-9 na Ufunuo
13:3-4.) Kwa nini, ndugu, usichague kusimama upande wa Bwana kwa kuzitunza amri zake na
kuishika Sabato yake? Je, jina lako linawezaje kuandikwa katika kitabu cha uzima cha
Mwanakondoo? Tafakari kisa hiki. Wakati Waisraeli walipozidi kumwasi Bwana jwangwani,
Mungu alimwambia Musa kuwa atawaangamiza Waisraeli halafu atamfanya yeye (Musa) kuwa taifa
kuu (soma Kutoka 32:9-11.) Lakini Musa akamsihi Bwana na kusema, “Walakini sasa ikiwa
utawasamehe dhambi yao na kama sivyo unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika”
(Kutoka 32:32.) Lakini “Bwana akamwambia Musa, mtu yeyote aliyenitenda dhambi ndiye
nitakayemfuta katika kitabu changu….” (fungu la 33.) Kwa hiyo mtu anayeandikwa katika kitabu
cha uzima cha Mungu ni yule aliyesamehewa dhambi (amekiri, ameungama na kuziacha) na
amehesabiwa haki. Na kama tulivyotangulia kujifunza, mdhambi anasamehewa au anahesabiwa haki
pale anapomkiri na kumwamini Bwana Yesu na hapo ndipo jina lake huandikwa katika kitabu cha
uzima (soma Matendo 2:38-39 na Warumi 3:21-26.) Kwa kuwa Kristo anapopokelewa moyoni
anatupatia uwazo wa kumtii Mungu kwa kuzishika amri zake, basi yeyote atakayempokea Yesu
ataonyesha utii kwa amri hizo. Hivyo utii mkamilifu kwa amri za Mungu utakuwa ngao dhidi ya
hatari ya kumsujudia Mnyama na sanamu yake.

Mungu wetu wa upendo ametufunulia mambo haya wazi. Kwa nini tupotee? Hebu mchague Yesu
leo na uamue kuishi sawasawa na amri zake ili jina lako liwe katika kitabu cha uzima, usije
ukamsujudu Mnyama badala ya kumsujudia Mungu.
- “Kunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu” - Ni hukumu ya kutisha, au adhabu kali
watakayopata wale wote watakaomsujudu yule mnyama (Roma). Ufunuo 15:1;16:1-21.
Wote watakaokataa kuupokea ukweli, watakuwa wamechagua adhabu hiyo.
- “Isiyochanganywa na maji” - Maana yake isiyo na huruma (soma Yakobo 2:13).
- “Kuteswa kwa moto na kiberíti” - Adhabu katika ziwa la moto (soma Ufunuo 20:10-15).
Wakati tunaelezwa juu ya wale watakaomsujudu mnyama na sanamu yake, tunaelezwa pia juu ya
watakatifu wa Mungu katika saa hii ya mwisho ambao neno la Mungu linasema watatambulikana kwa
kuzishika amri za Mungu na kuwa na imani ya Yesu, ishara kuu itakayowatambulisha ni kuitakasa na
kuitunza Sabato ya siku ya saba ya juma, yaani Jumamosi. Kumbuka Sabato ndiyo ishara ya Mungu
wa kweli aliye muumbaji.

Mpendwa msomaji, sasa tunasimama ukingoni kabisa mwa wakati wa kufungwa kwa rehema na
historia ya dunia hii. Ukweli wa neno la Mungu umefunuliwa wazi kwetu, kwa nini tusichague
kuokolewa sasa kabla hatujachelewa milele (soma 2 Kor. 6:2)? Usije ukadharau maneno haya kama
jambo dogo tu. Pima kila kitu kwa nuru ya neno la Mungu. Kabla ya kufika mwisho, napenda
nikukumbushe visa viwili vya pekee ili kukusaidia - Kisa cha kwanza ni uasi wa Adamu na Hawa.
Unajua kwa akili yetu, kula tunda ni jambo dogo sana, lakini je, matokeo haya mabaya na ya kutisha
yaliyoenea duniani leo unajua ni kutokana na hili lililoonekana dogo tu? Kisa cha pili ni wakati
Sodoma na Gomora ilipoangamizwa kwa moto. Baada ya Lutu na mkewe na binti zao wawili
kutolewa nje ya mji, walipewa sharti la kutotazama nyuma na kuwa yeyote ambaye angetazama
nyuma angeangamizwa pamoja na miji ile. Mke wa Lutu aligeuka nyuma na akawa nguzo ya chumvi
(soma Mwanzo 19:17,23-26). Kugeuka nyuma tu!! Hivyo mpendwa, hebu kwa neema ya Mungu,
iliyofunuliwa kweli kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu, tuzingatie ujumbe huu, tutubu, tufungue
mioyo yetu na kuupokea ukweli wa neno la Mungu na kumpokea Yesu mioyoni ili awe Bwana na
mwokozi wa maisha yetu binafsi, ili tupate kuokolewa tusipotee na dunia. Wito wa Mungu wa
mwisho unasema “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo
yake” (Ufunuo 18:4). Tokeni Babeli.

Mungu anakuita utoke Babeli ili upone. Je, utaitikia wito huo wa rehema? Yesu yu karibu mlangoni
kuja kuchukua wateule wake (soma Yohana 14:1-3).

Huu utakuwa ndio mwisho wa pambano au vita vile vilivyoanzia kule mbinguni kati ya Mikaeli
(Yesu) na malaika zake na Ibilisi na malaika zake, kwa hiyo, kumbuka kuwa uamuzi wowote
utakaoufanya utakuwa unakuweka upande wa mmoja kati ya hao majemedari wawili - Yesu au
Shetani.

Comments

Popular posts from this blog

LINDA SAANA MOYO WAKO KULIKO VYOTE ULINDAVYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-I

VINYWA VYA MOYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-2

Ufanye Nini Unapoumizwa Moyo Na Watu Wako Wa Karibu/ Jinsi Ya Kupokea Uponyaji kwa Moyo Ulioumizwa