MAMBO YA KUEPUKA ILI KUTUNZA MISINGI YA IMANI KABLA YA KUANZISHA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

.


1. Epuka kuanzisha mahusiano na mtu asiye amini. Ijue kwanza imani ya mtu kabla ya kuanza naye mahusiano ya uchumba. Malaki 2:10 - 11

Malaki 2:10-11
[10]Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?

[11]Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa BWANA aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni.

2. Epuka kuanzisha mahusiano kwa kufuata namna, au kawaida au desturi ya dunia hii au ulimwengu huu. Dunia wana mungu wao na sisi tulioamini tuna Mungu wetu kwa hiyo kawaida, namna na desturi zetu zinapingana na zao.

Walawi 18:30
[30]Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

Walawi 20:23
[23]Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.

Warumi 12:2
[2]Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

3. Epuka kuanzisha mahusiano bila kumshirikisha Mungu na Roho wake pamoja na mchungaji wako (kiongozi wako wa Imani).
(Wagalatia 6:6; Zaburi 32:8; 2 Nyakati 15:3.)

Mungu anaijua njia yako ya mahusiano; anakujua ni nini unahitaji, na kipi kinakufaa, kwa hiyo ni muhimu sana ukamshirikisha kabla ya kuchukua au kuanza hatua yo yote. Sikiliza na kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu na kumshirikisha mchungaji wako kwa ushauri na maelekezo ili hatua zako ziwe za uhakika na salama.

4. Epuka mazungumzo mabaya yatakayoharibu imani yako.

Mazungumzo mabaya uharibu tabia njema. Kwa kweli hasa katika kizazi hiki ambacho kila mmoja ni mjuzi wa maswala ya ndoa kwa mtazamo wake yeye, kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusiana na mahusiano, na mengi yao ni mazungumzo mabaya. Ukipita vijiweni, katika mitandao ya jamii nk. watu wanazungumzia mahusiano, sasa wewe epuka mazungumzo mabaya yanayopotosha imani yako na kukutoa kwenye misingi ya kiimani ili ubaki salama.

5. Epuka kuwafuata au kuwaiga au kujifunza kutoka kwa watu walioshindwa kuilinda imani yao unapotaka kuanzisha mahusiano.

Siku hizi wapo watu wanaojiita watumishi wa Mungu ambao kutokana na madhaifu na makosa yao wamehalalisha mambo hayo kuwa mafundisho. Wana ujasiri wa kufundisha wakihalalisha mambo yasiyo sahihi kuwa ni sawa tu yakifanywa. Epuka kuwafuata watu wa namna hii watakupoteza.

Hata hivyo, kwa upande mwingine ni muhimu wewe kutojihalalishia makosa ya mtu mwingine aliyotangulia kuyafanya yakawa ni halali na kwako eti kwa sababu wengine (waamini, watumishi na wachungaji) waliorudi nyuma waliyatenda na unaona kana kwamba hakuna shida yo yote. Ilinde imani, ni kati yako wewe na Mungu.

NINI HUTOKEA KIJANA ANAPOANZISHA MAHUSIANO NA KIJANA ASIYEAMINI.

1. Hupelekea vita ya miungu katika ulimwengu wa roho. Jambo hili hupelekea mahusiano ya uchumba hadi ndoa kuwa na mashindano katika ulimwengu wa roho na ndani ya kanisa. Mika 2:10 - 11

2. Hupelekea mashindano ya kiimani katika nafsi za wahusika na ndani ya kanisa (mwili wa Kristo) na hadi kwenye familia za wahusika.

Inapotokea wahusika wenye imani mbili tofauti (zinazopingana) wameanzisha mahusiano hapo ndipo migogoro huanza; muhusika yeye mwenyewe huwa na mgogoro na nafsi yake ndani yake, mgogoro wa yeye na kanisa au dini yake, mgogoro na wazazi wake. Sasa ili kukwepa yote haya na uwe na amani, anzisha mahusiano na mtu mwenye imani moja na wewe (aaminiye imani moja na wewe).

3. Asiye amini huwa mtego na mwiba kwa aaminiye na sababu ya kurudi nyuma.

Kutoka 34:12
[12]Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.

Ndoa ni agano; unapofanya agano na mtu asiyeamini (imani moja na wewe) mtu huyo huwa mtego kwako na ndiyo sababu Biblia imekataza kuoa au kuolewa na watu wasio amini.

4. Mungu anakuwa nje ya muunganiko huo; anajiweka pembeni ili aone mwisho wake. Unakuwa umefarakana na Mungu wako. Mika 2:10 - 12

5. Uwezekano wa kulitumikia kusudi la Mungu katika muunganiko huo unakuwa haupo.

6. Uhakika wa usalama wa ndoa na hali ya kudumu ya ndoa unakuwa haupo. Mahusiano yenu yanakosa uimara na uthabiti.

7. Uaminifu na utakatifu wa ndoa unakuwa haupo.

8. Adui wa mwenzi wako wanakuwa adui zako, roho zinazomtawala zinakutawala na wewe na mungu wake anakuwa mungu wako na kwa sababu hiyo anakuwa na uwezo juu yako.

Tutaendelea na sehemu ya pili ya somo letu. Ubarikiwe.

Na,
Mch. Ezekiel P. Bundala
0673184468

Comments

Popular posts from this blog

LINDA SAANA MOYO WAKO KULIKO VYOTE ULINDAVYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-I

VINYWA VYA MOYO: JINSI YA KULINDA MOYO WAKO-2

Ufanye Nini Unapoumizwa Moyo Na Watu Wako Wa Karibu/ Jinsi Ya Kupokea Uponyaji kwa Moyo Ulioumizwa